Okoa maisha ya mama na mtoto
“Saving lives of Mothers and Infants”

UTANGULIZI
Tanzania inakadiriwa kupoteza maisha ya kina mama wajawazito 578 kati ya 100,000 wanaojifungua na sababu zinazochangia ni pamoja na uhaba wa wataalam wa afya na ukosefu wa huduma ya dharura kwa wajawazito hususani katika ngazi ya vituo vya  afya na zahanati. Ni kutokana na hali hiyo, Taasisi ya Benjamin William Mkapa HIV/AIDS Foundation katika kuunga mkono juhudii za serikali katika kuboresha afya ya mama na mtoto hususani katika maeneo ya vijijini, imeanza utekelezaji wa mradi ujulikanao kama Okoa Maisha ya Mama na Mtoto kwa lugha ya kiingereza “Saving lives of Mother and Infant”.

LENGO LA MRADI:
Mradi umeanzwa kutekelezwa kuanzia mwezi Januari 2009, katika Wilaya za Iramba na Singida Vijijini zilizopo mkoani Singida, kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii chini ya ufadhili wa shirika la kimarekani la World Lung Foundation kupitia Taasisi ya Ifakara Health Institute (IHI). Kwa awamu ya kwanza, mradi umeanza kutekelezwa katika vituo viwili vya afya vya Ikungi kutoka Singida vijijini na Ndago cha wilaya ya Iramba. Lengo kuu la mradi ni kujengea uwezo wa vituo vya afya kutoa huduma ya dharura ya kumsaidia mama mjamzito ijulikanayo kwa lugha ya kitaalamu “Emergency Obstetric Care”.
Mradi unatarajia kutekeleza yafuatayo:

  1. Utoaji mafunzo kwa watoa huduma katika vituo hivyo vya afya ili waweze kupata stadi na mbinu za kumsaidia mama mjamzito ambaye anapatwa na dharura wakati wakujifungua.
  2. Kuhakikisha upatikanaji wa vitendea kazi (vifaa) vinavyosaidia kutoa huduma bora na muhimu wakati wa uzazi na kwa mtoto mchanga
  3. Kuboresha miundo mbinu ya vituo vya afya hususani uboreshaji wa majengo yanayotumika kwa ajili ya uzazi, yaani maternity ward.
Mama anahitaji mazingira mazuri wakati wa kujifungua (Ikungi Health Center). Katika hatua za mwanzo tayari mradi umeshaanza kutoa mafunzo kwa watoa huduma tisa(9),waliopo katika vituo vya afya, mafunzo ambayo yameendeshwa kwa wiki tatu(3) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Katika mradi huu, Taasisi imezingatia kushirikisha wataalam wa mikoa akiwemo daktari bingwa wa akina mama mkoani, pamoja na watalaam wa afya wakiwemo madaktari ambao wapo chini ya mradi wa Mkapa Fellows Programme. Mafunzo ya utoaji huduma ya dharura kwa wanawake wazazi na watoto Wauguzi wenye ujuzi wakimhudumia mama mjazito.

HITIMISHO:
Mradi wa Okoa maisha ya mama na mtoto, ambao upo katika awamu ya kwanza unategemewa kuwa mfano kwa wadau wa afya wanavyoweza kuimarisha vituo vya afya kutoa huduma ya dharura kwa wajawazito ili kupunguza vifo vitokanavyo na kukosekana kwa huduma hiyo.