Bodi Mpya ya BMAF

TAARIFA KWA AJILI YA VYOMBO VYA HABARI (PRESS RELEASE)

UZINDUZI WA BODI MPYA YA TAASISI YA BENJAMIN WILLIAM MKAPA HIV/AIDS FOUNDATION (BMAF) - 4 SEPTEMBA 2009


Taasisi ya Benjamin William Mkapa HIV/AIDS Foundation (BMAF) ni Asasi isiyo ya kiserikali (AZAKi),  iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria za usajili (Namba 375) mnamo tarehe 13, Aprili  2006. Taasisi hii ilianzishwa kwa ushirikiano wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Benjamin William Mkapa na Rais Mstaafu wa Marekani, Mh. Bill Clinton.

Mpango Mkakati wa miaka mitano (2008-2012) wa BMAF unalenga kuchangia nguvu katika kufikia Malengo ya Milenia (MDG’s), Mpango wa Taifa wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini Tanzania (MKUKUTA) na Mpango Mkakati wa Tatu wa Sekta ya Afya.

Dira ya Taasisi ni kuwa kitovu cha ubora katika mapambano dhidi ya UKIMWI katika ngazi mbalimbali nchini pamoja na kuboresha  maendeleo ya wataalam wa afya hususan katika maeneo yenye mazingira magumu.
Katika kuleta ufanisi wa utendaji kazi, Menejimenti ya Taasisi ya BMAF inasimamiwa na Bodi ya Wadhamini pamoja na Bodi ya Wakurugenzi. Bodi ya kwanza ya Wakurugenzi iliundwa Februari 2006 na muda wake wa utendaji wa miaka mitatu umefikia kikomo mwaka 2009.

Bodi hiyo ya kwanza kwa Taasis, yenye wajumbe wenye fani mbalimbali, iliweza kusimamia kwa ufanisi wa hali ya juu uanzishaji na uimarishaji wa mifumo kadhaa ya Taasisi hii, pamoja na kutoa miongozo madhubuti ya uendeshaji wa  programu za Taasisi. 

Menejimenti ya Taasisi ya BMAF inatoa shukrani za dhati kwa wajumbe wote wa Bodi kwa ushirikiano uliotolewa kwa kipindi chote cha utendaji wa kazi.

Kutokana na ukomo wa Bodi ya kwanza, Msarifu (Settler) wa Taasisi ya BMAF ambaye ni Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Benjamin William Mkapa ametua Bodi mpya ya wakurugenzi itakayoongoza kipindi kingine cha miaka mitatu (3).

Bodi mpya ya Wakurugenzi in wajumbe saba wafuatao :

  1. Meja Jenerali (Mstaafu) Herman Lupogo     - Mwenyekiti
  2. Mh. Abdulrahman Kinana                          - Mjumbe
  3. Bi. Caroline Temu Kavishe                         - Mjumbe
  4. Dk. Gilbert Ronald Mliga                            - Mjumbe
  5. Dk. Adeline Kimambo                               - Mjumbe
  6. Dk. Malick Juma                                      - Mjumbe
  7. Bw. Solanus Nyimbi                                - Mjumbe


Bodi hii imezinduliwa rasmi leo tarehe 4 Septemba, 2009 na Msarifu (Settler) wa Taasisi.  .

Kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini na Menejimenti yote ya BMAF, tunapenda kuwapongeza wajumbe wote walioteuliwa kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya BMAF. Tunaamini tutapata ushirikiano wao mzuri katika kufanikisha dira, dhima na malengo ya Taasisi hii. 

Dr. Ellen Mkondya-Senkoro
Mkurugenzi Mtendaji
Benjamin William Mkapa HIV/AIDS Foundation